Sunday, February 25, 2024

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano.

Kati ya matangazo hayo, tangazo la mkutano wangu wa tarehe 15 Februari mjini Faribault, Minnesota, lilitia fora.
 

Monday, February 19, 2024

MPIGA DEBE WANGU MPYA MAREKANI

Katika shughuli zangu za uandishi na kutoa ushauri kwa waMarekani na waAfrika kuepusha migogoro na matatizo mengine yatokanayo na tofauti za tamaduni, nina bahati ya kuwa na wapiga debe wa mataifa mbali mbali, wanawake kwa wanaume.

Mmoja ambaye amejitokeza miaka ya karibuni kama mpiga debe wangu ni Audrey Kletscher Helbling, mwanablogu maarufu wa hapa jimboni Minnesota. Alianza kunifahamu miaka michache iliyopita katika ushiriki wangu kwenye International Festival Faribault.

Wiki za karibuni amepata kusoma vitabu vyangu. Alianzia na Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences, ambacho alikiongelea katika blogu yake. Kwenye andiko lake hilo, alikuwa ananadi mhadhara wangu uliopangiwa kufanyika tarehe 15 Februari, 2024, mjini Faribault, jimbo la Minnesota.

Mdau huyu alihudhuria mhadhara ule na aliongelea vizuri sana katika blogu yake. Katika ujumbe wake huo, alinipigia debe, akahitimisha kwa kuwahimiza watu wasome vitabu vyangu, iwe ni kimoja au vyote.  Aliviorodhesha: Africans and Americans: Embracing Cultural DifferencesChickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences, na Matengo Folktales.

Inaniletea faraja na furaha kuwa na watu wa aina hiyo, wanaoona thamani ya kazi yangu kama ninavyoona mimi mwenyewe. Sifanyi kwa sababu yao, bali ni kwa maamuzi na mapenzi yangu mwenyewe, kama nilivyotamka katika video hii.

Video: Kipande cha Hotuba Yangu Books on Central


 Februari 15, 2024, nilitoa mhadhara mjini Faribault, jimbo la Minnesota, kuhusu tofauti za tamaduni baina ya waAfrika na waMarekani. Mhadhara ulifanyika katika duka la vitabu la Books on Central, na hapa naleta video ya kipande cha mhadhara, nikiwa nasoma paragrafu ya kwanza ya kitabu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences

Sunday, February 18, 2024

Mwanablogu Marekani Akichambua Kitabu cha "Chickens in the Bus"

Mwanablogu na mwandishi Audrey Kletscher Helbing wa Minnesota, Marekani, ambaye ni mfuatiliaji wa shughuli zangu za kuelimisha katika jamii, amechapisha uchambuzi wa kitabu changu Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences.  Soma hapa.

Saturday, February 10, 2024

Taarifa fupi ya Mhadhara Mjini Owatonna.

Tarehe 8 Februari, nilikwenda mjini Owatonna, hapa katika jimbo la Minnesota. Nilikuwa nimelikwa na mkurugenzi wa Owatonna Public Library kutoa mhadhara juu ya changamoto za tofauti za tamaduni baina ya waAfrika na waMarekani.

Mahudhurio yalikuwa makubwa, kwa mujibu wa mkurugenzi. Miongoni mwa wahudhuriaji alikuwa bwana Tim Penny ambaye aliwa kuwa mjumbe katika bunge la wawakilishi hapa nchini Marekani.

Mhadhara ulikwenda vizuri, na wahudhuriaji walikuwa na masuali ya kusisimua. Kikao kilipoisha, watu walinunua vitabu, na mmoja wao alikuwa bwana Tim Penny aonekanaye pichani. Aliwahi kuwa mjumbe katika Baraza la Wawakilishi la Marekani.

Sunday, January 14, 2024

Vitabu Vinaenda Iran

 Tarehe 12 Januari, 2024, nilisafirisha vitabu vyangu viwili, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences, kwenda Tehran, Iran, kwa mwendesha kipindi cha televisheni kiitwacho THE ENLIGHTENMENT SHOW. Hii ilikuwa ni baada ya yeye kufanya mahojiano nami, akiwa amelenga zaidi kwenye mada ya fasihi ya Afrika na ukoloni, na pia mitazamo ya waMarekani kuhusu Afrika.

Mahojiano tulifanya kwa Zoom, na hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kufanyiwa mahojiano Iran. Ninasubiri kwa hamu kupata mrejesho kutoka kwa watu wa kule, hasa baada ya vitabu vyangu kuwafikia.


Sunday, January 7, 2024

NIMEKABIDHI “CHICKENS IN THE BUS”

Januari 4, 2024, nilikwenda Maple Grove, kukabidhi nakala 20 za Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences kwa mama wa Cameroon ambaye alikuwa ameziagiza kwa ajili ya shule fulani nchini Cameroon.

Katika maongezi, mama huyu alinieleza habari za shule yenyewe, ambayo iko kaskazini magharibi mwa Cameroon, uliko mji wa Bamenda. Alinieleza kwamba lengo lake ni kuwa hivi vitabu visomwe na wanafunzi wa darasa la sita kwenda juu. 

Tuliongelea umuhimu wa kuwafundisha watoto wa kiAfrika juu ya utamaduni wetu, na kuwajenga katika kuuheshimu. Huyu mama alisisitiza kuwa yaliyomo katika Chickens in the Bus yanakidhi malengo hayo.

Mimi kama mwandishi nafurahi sana kujua kuwa watoto wa kiAfrika watakuwa wanasoma na kutafakari kitabu changu 
 

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...